Tuesday, December 6, 2011

MATARAJIO NA MAFANIKIO YA HARAKATI ZA ANTI VIRUS



Harakati za Anti-virus, matarajio, mafanikio na matatizo yaliyojitiokeza. 

Utangulizi:

Kwanza natanguliza shukrani zangu za dhati kwa waanzilishi wa harakati hizi zinazokwenda kwa jina anti – virus, hapa bila hiyana namtaja mh. Mbunge joseph Osmond mbilinyi maarufu kama ‘’sugu’’ pia danniel kamili ‘’danny msimamo’’, fredy malik ‘’ mgosi mkoloni’’, adili mkwela, g. solo, mapacha – maujanja saplayaz, isanga family, prof. ludigo, king kiboya, peen lawyer, rama dee, d wa getho, anselin tryfon Ngaiza ‘’soggy doggy’’, suma gangster, coin, zay b, sister p, times fm team, pia radio zinazosaidia harakati hizi, na wanaharakati wote bil kuwasahau wadau wenye mlengo na mchango chanya kupitia kurasa za mitandao ya kijamii hasa facebook hapa sitoweza kuwataja wote kwa majina maana ni wengi mno zaidi ya 100,000 hivi kwa hesabu ya haraka ambao kila mmoja anacheza nafasi yake kama mlinzi wa muziki kwa jinsi awezavyo kupitia michango yao katika groups kama I’m Swahili original, yes we can, magenge with attitude, hip hop forum 255 icon, anti-virus dawa ya virus wa muziki wa bongo na group nyingine nyingi zilizowiana sawa na hizi katika kufanikisha kuwa ujumbe unafika pia harakati zinaeleweka kwa jamii na kufanikiwa. Pia Watanzania wote ndani na nje ya Tanzania kwa mchango wao wa kuthamini na kukubali ni nini hizi harakati zinakusudia na kuhakikisha kuwa zinafahamika mbali zaidi na kufanikiwa kiukweli. Watu wote waliotajwa hapo juu na ambao hawajatajwa wamekuwa wakionesha ujasiri wa wazi pasipo uoga wa aina yoyote hii inaonyesha ukimya wao ulikuwa na kelele zaidi ya wanazozipiga sasa katika kutetea muziki huu wa bongo pia hiphop ndani ya Tanzania huru.

Anti virus ni nani?

hili ni swali kwa watu wengi wanofuatilia harakati hizi kwa njia na vyanzo mbalimbali, kama ilivyo katika kitarakilishi yaani kompyuta anti virus ni kitu kisicho shikika pia bebeka na huafanya kazi ya kuondoa virusi waharibifu katiaka kompyuta na kuiacha katiaka hali ya usalama zaidi wa kuiwezesha kuwa na kumbukumbu nzuri na spidi ya kutafuta mafaili na vitu vingine vilivyotunzwa katika kompyuta husika, vivyo hivyo maana inaingia moja kwa moja katika hizi harakati ambapo, anti virus inasimama badala ya wasanii wenye uwezo wa kufanya mziki walioamua kupingana na unyonyaji, uonevu, uchonganishi, ubaguzi, utumwa dhidi ya wadau wenye malengo binafsi na kazi zao na baadhi ya vituo vya radio na tv vinavyofanya ubaguzi huo na kuwanyonya wasanii hawa. Hawa wamejitoa muhanga kwa lugha ya kuscan na kudelete virusi wote ndani ya kiwanda cha muziki. Na ipo katika mfumo wa mixtapes.

Vinega ni nani?

Vinega ni wanaharakati wote wanaoheshimu utu wao na kazi zao kisanaa, kijamii, na kiuchumi pia. Hawa ni wale waliochoka kuvumilia unyonyaji unaondelea kukua kukua katika kiwanda cha sanaa. Hawa ni wale wasioogopo kumwambia meneja masoko kuwa wewe ni mwizi wala hawajashindwa kuwambia ma dj kuwa nyinyi sio ishu mnatubagua, pia hawajashindwa kwenda mbele na kuandika mashairi kwa ajiri ya kukosoa mifumo ya kinyonyaji inayoendelea dhidi ya wasanii mfano mimi ni kinega, sugu ni kinega, peen lawyer ni kinega, adili hisabati ni kinega, rama dee ni kinega, mgosi mkoloni ni kinega, danny msimamo ni kinega, soggy doggy ni kinega, d wa ghetto ni kinega, suma g ni kinega, hata wewe na yule ni vinega.

Magenge ni nani?

Hawa hawana tofauti na vinegar, kwani vinega wote ni magenge na magenge wote ni vinegar. Ndio maana utasikia maneno kama mgenge yamecharuka, magenge wamekinukisha.

Viwaki ni nani?

Viwaki hawa ndio hasa virusi wenyewe na wahujumu wa muziki (watangazaji, ma-dj, radio na tv, viongozi wanaohujumu muziki kwa namna moja au nyingine) wanofanya vinega na magenge wapate hasira za kuzianzisha hizi harakati za anti virus na kuzipeleka mstari wa mbele zaidi sio tu dar es salaam bali mikoa yote ikiwembo Mbeya, arusha, mwanza, iringa nk. Hapa utasikia maneno toka kwa magenge wakisema, ‘’usilete uwaki, umefua kiwaki. Hivyo ukiitwa kiwaki jua wewe ni virus na unatakiwa kuscaniwa.

Matarajio ya harakati za anti virus.

Katika kuanza kwake miaka ya 2010 na muendelezo wake mpaka sasa 2011 harakati hizi zimekuwa na matarajio mengi kufanyika ili kuweka malengo yake yafikiwe. Kuingiza mixtape mbili mtaani kwa kuzigawa bure kwa wadau hii ni kwa sababu ujumbe ulitakiwa uanze kusambaa haraka kwa jamii husika hususani wadau wa huu muziki walio nchini na nje ya nchi. Yafuatayo ni baadhi ya matarajio ya harakati za anti virus



Ø      Kufikisha ujumbe tarajiwa wenye mahitaji halali yalio muhimu, ujumbe huu umeelekezwa kwa watu wote wenye nia njema na mbaya na muziki na wasanii wake.

Ø      Kuleta ujasiri wa kudai haki za wasanii kwa wasanii wenyewe na wadau wa muziki ambao kwa kiasi kikubwa ni wasikilizaji na wateja wa muziki au sanaa husika.

Ø      Kuamsha walio lala na waliokata tama katika kudai na kufuatilia haki zao za msingi ambazo ziliwapelekea hata kupotezwa au kutopigwa kwa nyimbo zao radioni hata kwenye vituo vya tv mbalimbali.

Ø      Kuleta Umoja hai baina ya wasanii wakongwe na wageni katika kiwanda cha muziki ili wawe na sauti na nguvu moja kupigania haki zao pasipo kugawanywa katika makundi yanayodhoofisha hata uwezo wao kisanaa.

Ø      Kuondoa chechembe zote zinazoashiria unyonyaji na uonevu hata kwa vile vifaa au fungu linalogawiwa kutoka serikalini. Hapa lengo ni kwamba kila msanii na afaidi keki hiyo iliyo tolewa kwa uwiano sawa na wengine pasipo kuangalia hitikadi yake kisiasa, kikabila, kimkoa wala kidini.

Ø      Kuwasaidia wasanii wachanga wanaofanya mziki mgumu (hiphop) kutovunjwa moyo kwa kunyimwa promo bali kuwawekea mazingira ya kuona ni chaguo lao sahihi pia kujitokeza kwa wingi kufanya mziki huo pasipo kuingiliwa maamuzi yao.

Ø      Kuzishawishi radio na tv na watangazaji wake kutambua kuwa wasanii wanaumuhimu sana kwa mafanikio ya vyanzo hivyo vya habari na matangazo, hivyo waone umuhimu wa kuheshimu kazi za wasanii pamoja na kumtuza kile anachostahili pasipo kumpunja labda kwa kizingizio cha promo.

Ø      Kutengeneza daraja litakalo waunganisha wasanii na wadau wa muziki (wasanii, mashabiki na washika dau) pia serikali na wizara husika ili kuleta ukaribu utakao punguza mlolongo wa kutatua matatizo yao kwa amani.

Ø      Harakati hizi pia zinawakumbusha wasanii kujiona kuwa ni watu muhimu na wanaweza kufanya mambo makuwa katika kuijenga jamii na nchi kwa ujumla hivyo kuwaweka katika meli moja bahari moja na uelekeo mmoja.

Ø      Kuwakwamua wasanii katika dhiki ya fikra na fikra mgando kuwa bila promo za radio hawawezi kutoka pia bila kufuta matakwa ya wenye redio hutosikika, kitu ambacho sio cha kweli pia sio cha kukivumilia hata kidogo.

Ø      Kuzisambaza harakati hizi sehenu kubwa zaidi hasa Tanzania na mikoa yake, ambapo wasanii wake ndio hasa walio kata tama ukilinganisha na muda wanaoutumia katika kubuni na kuandika mashairi yenye upeo na mlengo chanya katika kujenga jamii husika.

Ø      Kutumia lugha kali na hii ni katika kukemea na kuonyesha ni jinsi gani wasanii wamechoka. Lugha hii kali ndio itaibua gumzo na maswali kama kwanini itumike lugha kali, bila shaka ni kuleta hisia na kuibua fikra upya za kulitazama suala hili la wasanii na sanaa zao kwa jicho la tatu na kujua nia na madhumuni sio kutukana bali kutekenya ukweli wa mambo na kuuweka wazi.

Kwa kutaja machache hayo yanazaa mengine mengi hasa ukiyapambanua kwa mojamoja pia ukitumia sanaa husika, aina ya muziki na aina ya msanii. Haya ndio hasa matarajio ya kuanzishwa kwa harakati hizi za anti virus. Ni matarajio yalio kuwa ndani ya akili na mioyo ya wahusika ambapo mwanzoni ilikuwa kama utani ha hadithi. Ndoto iliyodhaniwa kuwa inaotwa mchana na waharakati wa anti virus iliotwa usiku na hatimaye kutimia na kuwa ya ukweli (dream came true) mara baada ya umma wa watamzania kwa wingi wao uliodhihirisha kuwa wanao sapoti hizi harakati ni  wengi kuliko ilivyotarajiwa hata na wahujumu wenyewe ikiwa ni pamoja na baadhi ya wanyonywaji wenyewe ambao walionyesha usaliti pia woga kuhusika  katika hizi harakati wakiwa na sababu bianafsi na shurutia, huku wakidai kuwa labda wanalinda maslahi ya kuendelea kukandamizwa na kujaribu kurobby promo ya mda mchache na malipo ya mda kwa show zilizoandaliwa na wanyonyaji wenyewe. Ulikuwa ni usiku wa tarehe 26 novemba, 2011 pale katika viwanja vya chuo cha ustawi wa jamii, bamaga kijitonyama, katika uzinduzi wa mixtape ya anti virus vol ii. Yaliyo tokea pale ilikuwa hata ukihadithiwa unapata picha safi kuwa hakika harakati zimefunguka na wadau wamefunguka. Hapa wasanii wakongwe na wanaochipukia walionyesha ukamilifu wao na kuudhihirishia umma kuwa hawajachuja kama inavyo tetwa na baadhi ya vyombo vya habari hasa radio na tv. Matukio mengi yalitokea hapa ikiwa ni pamoja na hisia za wazi toka kwa mashabiki kwa kuonyesha ni jinsi gain wanahamasika, hata baadhi ya wahujumu (majina shimoni) walikuja hapo lakini sijui kwa lengo gain kwani nao walikuwa na sehemu ya kuwepo kwa siku ile na muda ule.

Mafanikio ya harakati za anti virus.

Japokuwa ni muda mfupi tangu kuanzishwa kwa harakati hizi za anti virus na mlengo wa kusaidia muziki na wasanii wa bongo ikibidi kuigwa na mataifa mengi hususani ya afrika mashariki yaani Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi ambako pia kuna vuguvugu la uhujumu kwa wasanii na sanaa zao japo hapa bongo (tanzania) ni kiwango cha juu sana. Harakati hizi zimefanikiwa kwa kiasi kibwa japo ndio kwanza zinaanza kuchanua. Mafanikio haya ni kama vile;
 

Ø      Kuandaa, kuhamasisha show kubwa ya uzinduzi na kuhakikisha kuwa inafanyika kwa nguvu ya wasanii bila mkono wa mameneja masoko wala wadau wengine kama mapromota waliozoeleka.

Ø      Kuleta Umoja wa nguvu kwa wasanii waliokuwa mbali na mic kwa muda mrefu ambao wengi wao radio na vituo vya tv ni kama vimewasahau hata kwa mchango wao katika kuukuza mziki wa bongo ambao ndio chanzo kikubwa cha mapato na mafanikio pamaoja na umaarufu katika vituo hivyo vya kurusha matangazo.

Ø       Kufikisha ujumbe tarajali Kwa umma wa Tanzania, serikali (Kamati ya bunge chini ya wizara husika), wadau wa muziki na mashirika mbali mbali yanayo jihusisha na sana.

Ø      Kuibua joto kali Kwa wahujumu na uozo wao katika kiwanda cha muziki na sehemu zote walipowekeza hujuma zao, ambapo kila jicho sasa lipo kwao na matarajio ni kwamba waitende haki au wajitoe kuwaacha wasanii na wadau wenye nia ya kuwasaidia kiukweli pasipo rushwa wala takrima ya aina yoyote.

Ø      Kuweka mambo bayana. Hapa ni jinsi ya shughuli nzima ya harakati ilivyoendeshwa na inavyoendeshwa kupitia kurasa za mitandao ya kijamii na groups zake, pia vituo vya radio amabvyo viko na msaada wa kweli kwa wasanii, wadau waliopo kwenye hizi harakati yaani vinega wamekuwa wazi wazi kueleza ukweli zaidi bila woga ili kuujuza umma uliodhania tofauti labda kwa kupotoshwa na warusha matangazo kwa mfumo usio na lengo la kujenga. Vinega walifunguka ipasavyo kueleza umma bila woga ambapo walijaribu kugusia hata matukio mbalimbali yalio shatokea kwao katika kuwakandamiza kimuziki lakini wameonyesha kuwa wako tayari kusimamia haki zao sasa. Zaidi kusimama katika ukweli na si vinginevyo ili kuutenga uongo na woga.

Ø      Kupata fursa ya mialiko sehemu mabalimbali ikiwa ni ndani na nje ya nchi ya Tanzania. Hapa ni mara baada ya ile show ya uzinduzi pale viwanja vya chuo cha ustawi wa jamii. Hii haija wahi kutokea kwa nchi yetu show kuandaliwa na wasanii kufanikiwa kwa kiasi kikubwa na baada ya hapo wadau kuwataka wasanii hao wakafanye show na sehemu zingine mikoani ili kuendeleza harakati.

Ø      Kufanikiwa kukusanya watu wengi kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania ikiwa ni pamoja na mkoa husika wa dar es salaam, pia Mbeya, Dodoma, arusha, mtwara, Morogoro, pwani, tanga, iringa na mwanza. Hii ni hamasa kubwa kwa wanaharakati na wadau wanaosapoti hizi harakati kuona kuwa kumbe hawapo upwekeni bal wapo farajani na hasa toka pande zote za nchi.

Ø      Kufanikiwa kuanza mchakato hai wa kuuandaa show za mikoa mingine kupleka harakati na ukweli juu ya yaliyomo katika kiwanda cha muziki na wasanii wake ikiwa ni sambamba na burudani kabambe toka kwao wasanii waliochoka kuonewa na kuhujumiwa.

Ø      Kuzishawishi media mabalimbali kuona kuwa harakati hizi ni halali pia zenye maslahi kwa watanznia, wasanii, sanaa zao na serikali kwa ujumla, hivyo kuthamini kazi za wasanii na wadau kuacha hujuma juu ya wasanii na kazi zao kwani kwa kufanya hivyo inazidi ongeza hisia kwa vinega kuwa hawataki kuiachia haki ya wasanii hivyo itafutwe kwa nguvu.

Ø      Kujenga na Kukuza Mtandao wa vinega na magenge kupitia sehemu mbalimbali pia kupitia njia mbalimbli, ambapo hata ukusanywaji wa habari na matukio na kusambaza habari inakuwa imerahisika kwa kiasi kikubwa.

Ø      Pia fanikio ambalo ni la wazi lakini linajificha ni kuwa harakati hizi tangu zilipoanza kupamba moto kumekuwa na wimbi la wasanii waliotelekezwa na baadhi ya media kuanza kuitwa na Kupata promo ya mda ili waweze kujiona wamo, na hilo limepelekea hata kwa uchche wao Kupata fursa ya kusema juu ya walipwe kiasi gani japo kwa mara ya kwanza katika historia yao ya usanii na wakasikilizwa, hivyo wasanii wachache walioonekana wakiwa na uoga walijipatia show-ajira na promo ya hata zile nyimbo zao ambazo hazikuwahi kupigwa basi kutokana na vuguvugu la harakati hizi za anti virusi walinufaika japo hawawezi sema kuwa ni hizi harakati ndio ziliwaweka pale kwa wakati ule, pia wajiandae kurudi katika msoto ule ule.

Ø      Pia harakati zimeibua udhurumaji unao fanywa na mameneja masoko hasa wanapo leta msanii toka nje ya nchi, japo haiwezekani kuwepo kwa uwiano juu ya malipo baina ya wasanii wa ndani na wa nje, katika hili wasanii wa ndani hunyonywa sana kwa kupewa pesa ndogo lakini kwa kazi kubwa na ushawishi wao mkubwa kwa mashabiki na mafanikio ya show zenyewe.

Haya ni baadhi ya mafanikio makubwa ambayo hayajawahi kutokea katika maisha ya muziki na wadau wake katika nchi hii ya Tanzania. Hizi harakati zimeweza kuonyesha kuwa wasanii wakikaa amoja wanaweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa sana kuliko pale wanapo tengana na kuwekeana chuki kwa visingizio visivyo na msingi huku wengine wakitumia umaarufu wao waliopata kwa njia ya promo kudis wale ambao promo imewapita kando kwa sababu mbalimbali, na wengine basi tu labda kwa kuwa na uelewa finyu juu ya haki zao za msingi huku wengine wakizongwa na woga, wengine wakielekezwa nini cha kufanya na wenye media na kusahau hulka zao binafsi na wengine basi tu ni ulimbukeni wao na kuendekeza njaa na kuona hizi harakati labda ni za kihuni au la.

Sambamamba na mafanikio pia kuna matatizo yanaendelea kujitokea na mengine yashajitokeza mwanzoni wakati hizi harakati zinaendelea, kwanza ikumbukwe kuwa muasisi wa harakati hizi alianzisha harakati hizi hata kabla hajaingia bungeni labda niseme wala hakujua kama atagombea, lakini ikawa mchana ikawa usiku huku hizi harakati zikiwa masikioni mwa watu kupitia anti virus mixtape vol I kwa kipindi kile ilikuwa inapatikana kwa blog ya dj choka na blog zingine za hapa bongo, watu wakiwa tayari wamesha isikis wamesha pima uwezo wa hizi harakati na uelekeo wake, nae mh. Joseph mbilinyi akatangaza nia ya kugombea Ubunge kwa tiketi ya chama cha demokrasia na maendeleo katika jimbo la Mbeya mjini, huku uchagu huo wa mwaka 2010 ukiwa wenye kila aina ya matukio mazuri pia mabaya yalio ambatana na hujuma za wazi, rushwa na uonevu wa aina tofauti tofauti hasa kwa waliotangaza nia za kugombea kwa tiketi ya vyama pinzani, basi changanya nah ii ya anti virusi watu wengi wakiwa wadau wa muziki hata wananchi walitegemea kuwa harakati hizi labda zinge muangusha na kumdhoofisha hapa ntafupisha kwa kusema sugu kweli ni sugu, alikomaa kuanzia kwenye kura za maoni akapita na mchakato wa kampeni nakumbuka siku moja nikiwa napita kwenye kampeni za mpinzani wake nilimsikia kwa masikio yangu akijaribu kupotosha umma kwa kusema wazi kuwa ‘’ msimchague huyo sugu, kwanza nilimfukuza shule, pia sio Mtanzania anaishi marekani, mara akaongeza kwanza anaimba nyimbo za matusi anatukana vyombo vya habari ndio maana hata wenzake hawajaja kumsaidia . . . ’’ nilicheka lakini sikutaka kuhoji zaidi kwani naelewa alitaka nini. Cha kufurahisha zaidi ni kwamba wanambeya walichanganya a harakati hizi za anti virus ambapo kipindi kile kila saluni mkoani pale ilikuwa ni mwendo wa ‘’ I wanna kill ryt now . . .’’ ambayo ni ngoma aliyoifanaya sugu mwenyewe katika ile anti virus vol I (kituko kingine hapa nilikuwa nasikiliza radio moja hivi kabla hata ya kampeni za uchaguzi nilisikia eti kuna jamaa kamshitaki sugu kisa amemtishia kumuua kwenye huo wimbo ambapo alichukuliwa na polisi na kwenda kuhojiwa lakini ilikuwa kesi-zuzu yani isiyo na akili) wanambeya walimjadili sugu kwa marefu na mapana na hivyo kuthibitisha kuwa sugu anafaa na hataogopa mtu katika kutetea haki za wanambeya, kwa msaada wa hali na mali toka kwa kaka mgosi mkoloni, danny msimamo, isanga family (showkaz), g. solo, king kwaxa, gwano, dr. levy ambao naweza sema kweli walikuwa wakazi wa Mbeya tangu kampeni mpaka sugu anakabidhiwa jimbo usiku ule kwa mbinde na mikwara toka kwa polisi na mabomu kwa wingi huku tukiambiwa tutoke kimya kimya bila kushangilia na kila mtu aelekee kwao. Ni mengi yaliyo jiri kipindi kile cha kampeni, wapo walio hoji kuwa ‘’hivi watu wa Mbeya kweli wanaweza kumchagua msela?’’ huku baadhi ya vyombo vya habari hasa radio zikijaribu kubadili mfumo wao wa matanagazo na kuweka ugombea wa sugu kama ndio topic kila asubuhi huku wakijaribu kuweka kila aina ya mashambulizi lakini hawakuweza kuzibadili nafs za wana Mbeya na mgombea ambaye ni juzi tu wamemtunuku jina ‘’ rais wa mbeya’’. Alipoingia bungeni na imani kuwa hata wale wasanii waliodhani asingeweza walijua tayari wamepata mtetezi wa haki zao. Kwa kusema kweli homa ya matumbo Sugu kuwemo ndani ya nyumba ya kutungia sheria. Japo kuwa ni lulu na tumaini la wana Mbeya pia sugu anatizamiwa na wadau wa muziki hasa wanamuziki wenyewe ia wateja wa muziki kuwa atafanya mabadiliko aliyokuwa nayo tangu anaanza muziki enzi zile. Siamini ila nasema katika msafara huu wa mamba hata kenge wanajaribu kuingia tu kwa kujivika ngozi ya kondoo ilihali wakiwa na vitambulisho vya uchui.

Ni ada kuwa kila mafanikio huja kwa vikwazo ikibidi huja sambamba au mkabala na matatizo mbalimbali, hapa situkuwa mwingi wa maneno bali ntaenda moja kwa moja kwenye kile nilichokiona kwa macho yangu, nilichokisikia kwa masikio yangu na nilichohisi kwa hisia zangu sambamba maoni ya wanaharakati walioko mabalia na karibu yangu tangu walipoanza kuzifuatilia harakati hizi za anti virus ambapo kwa kutumia vyanzo vya maoni, katika kipengele hiki wengi nami nikiwemo tumetizamia kuwa japo matatizo ni mengi ila yafuatayo yanapewa nafasi kuzungumziwa,

Ø      Kuamini kwa kuona zaidi, hili ni tatizo kubwa lililojitokeza huku likichukua sura mpya kila kukicha na Kupata promo ya kuelezewa karibu katika kila palipo na wanaharakati wenyewe, hapa ni kwamba kuna baadi ya wasanii walikurupuka kuja na kujiunga na vinegar hasa kipindi cha vikao vya maandalizi ya show, lakini mda mchache wasanii hao walioaminiwa kwa macho kuwa wanasapoti hizi harakati wakasikika wakiongea maneno ya kejeri na kashfa kudhoofisha harakati, baadhi wakiwa wamepewa hata air-time katika baadhi ya nyimbo za anti virus  kwa kutajwa majina kuwa wanasapoti hizi harakati kumbe bado waoga na hawako tayari, hili limeumiza wengi na linaendelea kuwatafuna wengi kwa kukosa majibu ya swali ‘kwanini walimuamini kiasi kile kipindi kile!!?’ wasanii hao walijitoa na kuziacha harakati huku wakiwa ni wahanga  pia. Hapa tatizo lilojitokeza ni kwamba kuamini mtu haraka haraka bila kumtrace upeo wake kiharakati ndio kubeba na wasaliti ambao mwisho wa siku tunabakia midomo wazi kwa kauli zao mbele ya wahujumu wa muziki ambao ndio hasa virus na vieaki wa muziki.

Katika matatizo ntaishia hapo kwani hili ndio tatizo lililo jitokeza kwa kipindi hiki, huu walaka ni toleo la kwanza, nataraji kutoa toleo lingine kwa kila show itakapofanyika. Hii ni katika Kupata kitu cha kuhifadhi kwa kumbukumbu za baadae na kijivunia kwa ushahidi sio tu wa makofi bali wadau kusoma nyaraka za maandishi na kujua harakati zinaendaje. Hapa tutaweza hata kuwaeleza wadau kwa nguvu kwani tuna store ya matukio yetu katika kutetea haki za wasanii wa bongo.

Maoni:

Ø      Kutokana na wadau kuelewa kuwa harakati hizi zinahitaji sana uwepo wa mashabiki hivyo kuwe na ukaribu baina ya vinega wakubwa na wale ambao ni chipukizi ili kuwapa moyo pale wanapofanya hizi harakati kwa njia mbalimbali.

Ø      Kuna umuhimu wa kufikilia njia mbadala ya kuwepo kwa radio na kituo cha tv vikiwa chini ya vinega ili kuongeza nguvu ya kusambaza hizi harakati kwa haraka zaidi kabla adui haja fanya lolote na fikra zake mgando. Hii itasaidia kupromote kazi za vinega na magenge wasanii wengine,

Ø      Kwa baadae harakati zitakapo noga zaidi kuna umuhimu wa kujisachi na kujiona kuwa tunaweza kwa kufanya mpango wa kuwa jukwaa kwa ajili ya show na matamasha mabalimbali, hapa itasaidia kuwafikia mashabiki wa pande zote pasipo kujali upatikanaji wa jukwaa la kukidhi mahitaji.

Ø      Vinega na magenge kuna umuhimu wa kujenga utaratibu wa kutembelea vikundi halali vya sanaa na kujaribu kukaa nao na kufahamishana zaidi juu ya maisha na sanaa. Hapa tutajenga uhusiano mzuri na wadau wengi na kuwa na uwanja mpana wa kufanya mabo makubwa zaidi.

Ø      Kufungua studio itakayo weza saidia vinega kurecord na kutunza nyimbo zao kwa matumizi ya badae zikiwa tayari kwenye soft copy. Hapa vinegar wadogo ambao pia wana conscious kama za vinega wakubwa watapata fursa kufanya kazi zitakazo tumika katika harakati mbalimbali.

Ø      Kuongezwe kwa product za vitu kama t-shirts, sculfs, ribbon, magazine, pia culture mbalimbali zenye nembo za vinega na magenge kwa design mbalimbali.

Hitimisho:

Lazima tutambue kuwa baada ya show ya tarehe 26 novemba 2011 pale viwanja vya chuo cha ustawi wa jamii, umma na watanzani walipata ujumbe moja kwa moja kuwa ni nini kinchofanyika katika harakati hizi. Tukumbuke kuwa watu wengi wamejitoa kusaidia hizi harakati kwa hali na mali pia kwa njia mbalimbali. Hii inaleta hamasa na faraja kubwa sana kwa vinega na magenge wa harakati hizi, tuzidi kushirikiana, tuzidi kupendana pia tuzidi kumuomba Mungu azidi kujaza kudra na Baraka zake ili asitokee wa kuturudisha nyuma kwa namna yoyote ile. Tudumishe team work style katika kufanya kazi za harakati na za kisanaa. Tujaribu kuangali wenzetu wa nje walio unganisha nguvu zao pamoja wanavyofanikiwa, tumejaliwa wingi wa vipaji ndani ya nagenge na vinega, tuna maproducer wakali wa kutosha, wasanii wakali wa kutosha, wabunifu wazuri, pia waandishi wazuri hivyo kufanya kazi kwa pamoja (collaboration) itaongeza morally kwa wadau wanaosapoti hizi harakati na wanaharakati wenyewe. Pia tutambue kuwa mh. Mbunge angeweza kusema basi kwani tayari ni Mbunge na ana majukumu ya kiserikali, lakini bado yupo nasi huku na huko tena vichochoroni katika kuwawinda wahujumu wa huu muziki, hapa natoa angalizo kuwa tusimwangushe anahitaji sapoti yetu ili kuitimiza ile adhma yake ya kuwasaidia wasanii ili nao waonje utamu wa keki ya jasho lao ambalo ni kipindi sana inaliwa na watu hata wasiojua msanii anaumizaje kichwa na anapataje pesa mpaka anarecord wimbo ukahit. Nguvu na Umoja wetu utamfanya mh. Mbunge Sugu ajione kuwa yupo na watu wanaomsapoti, hapo tunaweza pia kuomba akayazungumze zaidi mjengoni ili kuhakikisha wahujumu wanafungasha virago.



Mungu zibariki harakati za anti virus.

Mungu wabariki vinega.

Mungu ibariki Tanzania.





Imeandikwa na;



Real Hustlanomic. (Kinega)







(my GOVERNMENT my HEAD my NATION my BED)

1 comment:

/>